Numbers 3:23-38

23 aUkoo wa Wagershoni walitakiwa kuweka kambi zao upande wa magharibi, nyuma ya Maskani. 24Kiongozi wa jamaa za Wagershoni alikuwa Eliasafu mwana wa Laeli. 25 bKatika Hema la Kukutania, Wagershoni walikuwa na wajibu wa kutunza Maskani na hema, vifuniko vyake, pazia katika mlango wa kuingilia ndani ya Hema la Kukutania, 26 cmapazia ya ua, pazia katika ingilio la ua unaozunguka Maskani na madhabahu, pamoja na kamba, na kila kinachohusika kwa matumizi yake.

27 dKwa Kohathi kulikuwepo koo za Waamramu, Waishari, Wahebroni na Wauzieli; hizi ndizo zilizokuwa koo za Wakohathi. 28 eHesabu ya waume wote wenye mwezi mmoja au zaidi ilikuwa watu 8,600. Wakohathi waliwajibika kutunza mahali patakatifu. 29 fKoo za Wakohathi zilitakiwa kuweka kambi zao upande wa kusini wa Maskani. 30 gKiongozi wa jamaa za koo za Wakohathi alikuwa Elisafani mwana wa Uzieli. 31 hWaliwajibika kutunza Sanduku la Agano, meza, kinara cha taa, madhabahu, na vile vyombo vya mahali patakatifu vinavyotumika kuhudumu, pazia, na kila kitu kinachohusika na matumizi yake. 32 iKiongozi mkuu wa Walawi alikuwa Eleazari mwana wa kuhani, Aroni. Aliwekwa juu ya wale waliowajibika kutunza mahali patakatifu.

33 jKwa Merari kulikuwa na koo za Wamahli na Wamushi; hizi zilikuwa koo za Merari. 34Hesabu ya waume wote wenye umri wa mwaka mmoja au zaidi waliohesabiwa walikuwa 6,200. 35 kKiongozi wa jamaa za koo za Wamerari alikuwa Surieli mwana wa Abihaili; hawa walitakiwa kuweka kambi zao upande wa kaskazini mwa Maskani. 36 lWamerari waliwekwa kutunza miimo ya Maskani, mataruma yake, nguzo, vitako na vifaa vyake vyote na kila kitu kilichohusika na matumizi yake, 37 mna pia nguzo za ua unaozunguka pamoja na vitako vyake, vigingi vya hema na kamba zake.

38 nMose, na Aroni na wanawe walitakiwa kuweka kambi zao mashariki mwa Maskani, kuelekea mawio ya jua, mbele ya Hema la Kukutania. Wao walihusika na utunzaji wa mahali patakatifu kwa niaba ya Waisraeli. Mtu mwingine yeyote aliyepasogelea mahali patakatifu angeuawa.

Copyright information for SwhNEN